IQNA

Siku ya Quds

Ayatullah Khamenei: Siku ya Quds mwaka huu itakuwa uasi wa kimataifa dhidi ya utawala ghasibu wa Israel

13:04 - April 04, 2024
Habari ID: 3478630
IQNA-Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema siku ya Quds mwaka huu itakuwa uasi wa kimataifa dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na kuongeza kuwa: "Utawala wa Kizayuni wa Israel utazabwa kibao usoni kutokana na shambulio lake dhidi ya majengo ya ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria, mapema wiki hii."

Katika hotuba yake kwa maafisa wa utawala wa Iran na matawi mengine ya serikali jioni ya jana Jumatano, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema shambulio hilo halitaweza kuinusuru Israel huko Gaza ambako imekuwa ikiendesha vita kwa karibu miezi sita dhidi ya Wapalestina.

"Juhudi za mfamaji za utawala wa Kizayuni kama ulivyofanya huko Syria hazitauepusha kushindwa. Bila shaka utazabwa kibao kwa hatua hii,” amesema Kiongozi Muadhamu.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa hakuna uwezekano wa kuwaokoa Wazayuni kutoka kwenye mtego walionasa ndani yake na kuongeza kuwa: Utawala wa Kizayuni utazidi kuwa dhaifu siku baada ya siku na kukaribia kudidimia na kuangamizwa, na tunatumai kuwa vijana wetu wataiona siku ambapo Quds Tukufu itakuwa katika milki ya Waislamu wakiswali hapo na ulimwengu wa Kiislamu utasherehekea kuangamizwa kwa utawala huo ghasibu."

Amesema maandamano yaliyopangwa kwa ajili ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu ambayo yataadhimishwa tarehe 5 Aprili katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, yatawakusanya watetezi wa Palestina sio tu katika nchi za Kiislamu bali pia katika nchi zisizo za Kiislamu ambazo zimekuwa zikipigania kukomesha uvamizi wa Israel dhidi ya Gaza.

"Siku ya Quds mwaka huu itakuwa uasi wa kimataifa dhidi ya utawala ghasibu wa Israel," amesema Kiongozi Muadhamu.

Ayatullah Khamenei amezitaja jinai zinazofanywa na utawala wa Israel huko Gaza ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari na mashambulizi dhidi ya wanawake, watoto, wagonjwa na hospitali kuwa “hazina kifani katika historia” na kusema Uhalifu huo ni mkubwa kiasi kwamba hata watu waliolelewa katika tamaduni za Kimagharibi huko Ulaya na Marekani wanapaza sauti kupinga jinai hizo.

Amesema Wazayuni wameshindwa kufikia lengo hata moja kati ya malengo waliyotangaza mwanzoni mwa vita dhidi ya watu wa Gaza mwezi Oktoba mwaka jana licha ya kupata misaada na uungaji mkono wa kijeshi, kifedha na kisiasa wa Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Walitaka kuangamiza Muqawama hasa kundi la Hamas, lakini hii leo Hamas, Jihad Islami na Muqawama wa Gaza unaendelea kutoa vipigo kwa utawala huo dhalimu licha ya mashaka yaliyopo.

3487803

Habari zinazohusiana
captcha